Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Saffar aliyasema hayo Jumanne, Oktoba 20, 2026, alipofanya ziara ya kuaga kwa Mufti wa Uganda, Mhe. Dkt. Sheikh Shaban Ramadhan Mubaje, katika makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda (UMSC), Kampala, wakati muda wake wa kulitumikia taifa hilo ulipokuwa ukimalizika.
Balozi huyo aliambatana na maafisa wakuu wa ubalozi, akiwamo Bw. Rezaeri, D. Ali Asghar, Mshauri wa Utamaduni; Bw. Muhsen Aghaloo, Katibu wa Kwanza; Bw. Luyimbaazi Issah Katungulu, mtaalamu wa masuala ya utamaduni; pamoja na Sheikh Yousuf Zubair Sserunjogi.
Katika hotuba yake, Saffar alimshukuru Mufti pamoja na wananchi wa Uganda kwa mapokezi mazuri na ushirikiano alioupata wakati wa kukaa kwake nchini humo, alisema: “Asante, Mheshimiwa Mufti, kwa ukarimu mkubwa ulionionyesha”.
Saffar pia alizungumzia mzozo unaoendelea katika Ghuba ya Uajemi. Alilitaja shambulio dhidi ya Iran kuwa ni kitendo cha uchokozi, huku akisisitiza kwamba hatua zilizochukuliwa na nchi yake zilikuwa za kujilinda na zilizingatia sheria za kimataifa kuhusu mamlaka na uhuru wa mataifa.
Alikumbusha pia nafasi ya Uganda kama mwenyekiti wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), ambayo Uganda na Iran ni wanachama. Alisema nchi hizo zinaweza kutumia ushirikiano wao wa kidiplomasia kama msingi wa kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati yao.
Balozi huyo anayemaliza muda wake alibainisha fursa zilizopo za kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kubadilishana utamaduni, sayansi na elimu. Alisema Iran iko tayari kushirikiana na Uganda kwa kubadilishana tafiti, maarifa, ujuzi na utaalamu unaoweza kuchangia mabadiliko ya kijamii na maendeleo ya kitaifa ya Uganda.
Alisema baadhi ya kampuni za Iran tayari zinafanya kazi nchini Uganda, huku nyingine zikivutiwa na fursa za uwekezaji, hasa katika sekta ya kilimo. “Tayari kuna kampuni kadhaa za Iran zinazofanya kazi nchini Uganda, na nyingine zaidi ziko tayari kuchunguza fursa za uwekezaji katika maeneo ya kilimo, kama vile kilimo cha mazao yenye mbegu za mafuta na ufugaji, kutokana na upatikanaji wa ardhi, hali nzuri ya hewa na rasilimali nyingine za asili,” alisema.
Saffar pia alisisitiza utayari wa Iran kuwapokea wanafunzi zaidi kutoka Uganda katika taasisi zake za elimu ya juu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza ushirikiano wa kitaaluma na kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Majibu ya Mufti
Kwa upande wake, Mufti Mubaje alitoa rambirambi zake binafsi kwa Balozi Saffar kufuatia kifo cha baba yake hivi karibuni. Pia alimpongeza kwa huduma alizozitoa kwa niaba ya Iran na wananchi wake katika kipindi cha uwakilishi wake nchini Uganda.
Mufti aliishukuru Serikali ya Uganda kwa kuendeleza ushirikiano wa pande mbili na Iran, pamoja na kuheshimu uhuru wa dini. “Sisi Waislamu pia tunaishukuru Serikali kwa kutupatia, kama ilivyo kwa makundi mengine ya kidini, uhuru wa kuabudu na kutekeleza imani yetu,” alisema Mubaje.
Aidha, alieleza kuthamini kwake uhusiano wa karibu ambao Balozi Saffar alikuwa nao na Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda, wakati wa utumishi wake nchini Uganda. Alisema: “Tunakutakia kila la heri katika majukumu yako mapya, kwa kweli tutakukosa". Mufti Mubaje pia alizihimiza pande zinazohasimiana katika mzozo unaoendelea katika Ghuba ya Uajemi kutatua tofauti zao kwa njia ya amani.
Naibu Mufti, Mhe. Sheikh Muhammad Ali Waiswa, pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Wanawake Waislamu, Mhe. Hajjat Sophie Saffina Kenyangi, pia walimpongeza Balozi Saffar kwa uongozi wake na kwa msaada alioutoa kwa wananchi wa Uganda katika kipindi chake cha utumishi.

Baadaye, Sheikh Mubaje alimkabidhi Saffar zawadi za kumbukumbu zenye nembo ya Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda, kwa kutambua huduma na ushirikiano wake na taasisi hiyo ya Waislamu.
Miongoni mwa viongozi wengine waandamizi wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda, waliohudhuria hafla hiyo ni Mhe. Dkt. Sheikh Hafiz Muhammad Harunah Bukenya, Naibu Mufti wa Pili, na Hadji Abbas Muluubya Ssekyanzi, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda.
Kabla ya kuondoka nchini Uganda, Saffar alishiriki katika kipindi cha mahojiano ya moja kwa moja kilichorushwa na Radio Bilal, inayomilikiwa na Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda, ambapo aliwaaga wananchi wa Uganda kwa ujumla.


Maoni yako